Takukuru yaendelea kusubiri kuwasilisha ushahidi dhidi ya Wana CCM
MWANZA
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru), Mkoa wa Mwanza imewaweka kiporo viongozi na makada wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) baada ya kuahirisha kutoa taarifa ya uchunguzi dhidi yao
iliyopangwa kutolewa Januari 15.
Wanaochunguzwa kwa
tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa wakati wa mchakato wa uchaguzi
ndani ya CCM ni pamoja na katibu mwenezi wa CCM Wilaya ya Ukerewe, Nicholaus
Munyoro; diwani wa Kata ya Murutunguru, Musa Manka; diwani wa Kata ya Bukindo,
Gabriel Gregory na Steven Mazige ambaye ni mwenyekiti wa CCM Kata ya Ukerewe.
Makada hao walitiwa
mbaroni na Takukuru Desemba 2, 2017 wakati wa mchakato wa uchaguzi wa viongozi
wa CCM mkoani Mwanza uliofanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba kwa madai ya
kukutwa wakigawana Sh400, 000 zilizosadikiwa kuwa rushwa iliyotolewa na mmoja
wa wagombea.
Akizungumza kwa njia ya
simu jana kuhusu suala hilo, mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Ernest Makale amesema
taasisi hiyo itapanga siku nyingine ya kutoa taarifa ya uchunguzi dhidi ya
viongozi hao baada ya kushindwa kufanya hivyo Jumatatu iliyopita.

Comments
Post a Comment