Nabii Tito awekwa kikaangoni na Serikali
Mkurugenzi
wa Idara ya Huduma za Sheria wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Marlin Komba amesema
hamtambui mtu anayejiita nabii Tito na kwamba hajasajili kanisa lake katika
ofisi ya msajili wa taasisi za dini.
Komba amesema Serikali imeona vitendo
anavyovifanya ‘nabii’ huyo kupitia mitandao ya kijamii na imeanza kuchukua
hatua.
“Ninachoweza kusema ni kwamba hakuna mtu
anayezuiwa kuongea hapa nchini, mwache aongee anavyoweza ila Serikali imeshaona
anachokifanya na yanayoendelea mitandaoni hatua zinachukuliwa dhidi
yake,” amesema Komba.
Kwa upande wao viongozi wa dini
wameonyeshwa kukerwa na kulaani vitendo anavyovifanya mtu huyo anayejiita nabii
na kusisitiza kuwa hakuna dini inayoruhusu hayo.
Msaidizi wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili
la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Chediel Lwiza
amesema kwa vitendo anavyofanya mtu huyo hapaswi kujiita mtumishi wa Mungu.
“Huyo hawezi kuwa mtumishi wa Mungu na wala
hafanyi huduma ya kanisa ni vyema watu kama hawa wafuatiliwe na hatua za
kisheria zichukuliwe dhidi yao. Natumaini Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo ndani
yake ina ofisi ya msajili wa taasisi za dini itafanya kazi yake.”
Lwiza ametumia fursa hiyo kuwasisitiza
Watanzania kwenda kwenye makanisa ya kweli yanayozingatia neno la Mungu.
Amesema, “Hakuna sababu ya kutangatanga,
Watanzania mkasali kwenye makanisa yanayotambulika na yanayosimamia na
kufundisha neno la Mungu. Kuhangaika ndiko kunakowafanya wengine waangukie kwa
watu kama hao. Wapo wanaojaribu kupotosha neno la Mungu lakini ukweli ni kwamba
neno la Mungu halipotoshwi.”
Hilo limeungwa mkono na Msemaji wa
Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Rajab Katimba ambaye amesisitiza
Serikali na viongozi wa dini kuingilia kati suala hilo.
Amesema hakuna kitabu chochote cha dini
kinachohamasisha ulevi na ukosefu wa maadili.
“Hilo suala linakwenda tofauti na dini na
mila na desturi zetu pia. Dini zinatakiwa kuleta amani na kuhamasisha watu
waheshimiane si kuzungumza mambo yanayokiuka maadili yetu. Naona ipo haja ya
viongozi wa dini na Serikali kuingilia suala hili na waende mbali zaidi kwa
kuongea naye huenda hafahamu anachokifanya.”

Comments
Post a Comment