LOWASSA ATINGA IKULU
Rais John
Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na waziri mkuu mstaafu, Edward
Lowassa, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Taarifa
iliyotolewa leo Jumanne na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson
Msigwa imesema kuwa baada ya mazungumzo hayo Lowassa amempongeza Rais Magufuli
kwa kazi nzuri anayoifanya na ametaja baadhi ya maeneo ambayo kazi kubwa
imefanyika kuwa ni kutoa elimu bila malipo, ujenzi wa mradi wa uzalishaji wa
umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge), ujenzi wa viwanda na ujenzi wa reli kwa
kiwango cha kisasa (Standard Gauge) ambavyo
vinazalisha ajira nyingi kwa Watanzania.
“Nimepata
faraja sana kuja hapa Ikulu kuonana na Mhe. Rais, tumezungumza nae na
nimempongeza kwa kazi nzuri anayoifanya, lazima tukiri anafanya kazi nzuri na
anahitaji kutiwa moyo.
“Moja
kubwa ambalo ni la msingi sana ni la kujenga ajira, katika kuanza ujenzi wa
reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro hapo anajenga ajira, na kwenye nchi
yoyote inayoendelea suala muhimu ni kujenga ajira, Stiegler;s Gorge ni kujenga
ajira na mingine ya aina hiyo, lazima kuwepo na kipaumbele cha kusema kwamba
tunajenga ajira, jingine ni la elimu, ni muhimu sana, hauwezi kuacha elimu
katika mambo yako unayofanya, hili nalo lazima lisemwe vya kutosha, kwa kweli
nakushukuru Mhe. Rais, you made my day,” amesema
Lowassa.
Kwa upande
wake Rais Magufuli amempongeza Lowassa kwa kutambua kazi kubwa inayofanywa na
Serikali na amesema ni mmoja wa viongozi ambaye kwa wakati wake ametoa mchango
wake katika nchi.
Rais
Magufuli ameongeza kuwa Lowassa ni mwanasiasa mzuri kwani hata wakati wa
kampeni za uchaguzi mkuu uliopita ambao naye aligombea kiti cha urais, hakuwahi
kumtukana.
“Mhe.
Lowassa ameniomba mara nyingi nikutane nae, na leo nimekutana nae, tumezungumza
mambo mengi, ameniambia ya kwake na mimi nimemwambia ya kwangu, kwa ujumla Mhe.
Lowassa ni mwanasiasa mzuri na tuendelee kuwaenzi wazee hawa ambao kwa nyakati
fulani walifanya mambo mazuri na mimi napenda kumpongeza Mhe. Lowassa ambaye
kama alivyosema hapa kuwa tumefanya mambo mazuri mengi.
“Ametaja
miradi mbalimbali tunayotekeleza, ametaja mradi wa Stiegler’s Gorge
utakaogharimu zaidi ya Shilingi Trilioni 7, amezungumzia juu ya elimu bure,
amezungumzia juu ya maji ambayo kwa bahati nzuri yeye alikuwa Waziri wa Maji na
anafahamu sasa tumefikia wapi, amezungumza juu ya umeme tulivyosambaza katika
vijiji mbalimbali, elimu bure, huduma za hospitali na mengine,” amesema Rais
Magufuli.

Comments
Post a Comment