AFRIKA YATAKA TRUMP AOMBE RADHI KWA KUITUSI
Nchi 54 za Afrika zimemtaka Rais wa Marekani Donald Trump kuziomba radhi
baada ya kuripotiwa kutumia maneno machafu alipokuwa akizungumzia kuhusu
wahamiaji kutoka mataifa ya Afrika, Haiti na El Salvador wakati alipokutana na
wabunge kwenye Ikulu.
Baada ya kikao cha dharura cha mabalozi wa nchi za
Afrika katika Umoja wa Mataifa, mabalozi hao wamesema wanatiwa wasiwasi na
mtindo unaozidi kujitokeza kwenye utawala wa Marekani wa kuwadunisha Waafrika
na kulaani vikali matamshi ya kibaguzi, ya kudunisha na ya chuki dhidi ya
wageni yaliyotolewa na Rais Trump.
Rais Donald Trump amekanusha kutumia maneno machafu juu
ya nchi kadhaa ikiwa pamoja na za Afrika. Trump aliuliza kwa nini Marekani
iwapokee wahamiaji kutoka nchi za uozo kama za Afrika, Haiti na El Salvador.
Kauli ya Trump imesababisha ghadhabu na mshtuko. Umoja wa
Afrika pia umemshutumu Trump kwa matamshi yake umesema umeshtushwa na
umesikitishwa na umemtaka Trump aombe radhi.

Comments
Post a Comment