Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema uwepo wa uchumi imara na unaokua kwa kasi ni miongoni mwa vigezo vinavyochangia ukuaji wa haraka wa sekta ya fedha nchini.
Mh. Majaliwa ametoa kauli hiyo leo mchana wakati akizindua Mpango wa Pili wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Jijini Dar es Salaam. Mpango huo unatarajiwa kutekelezwa kuanzia mwaka 2018 hadi 2022.
“Uwepo wa uchumi imara, miundombinu muhimu iliyojengwa na inayojengwa na Serikali pamoja na sekta binafsi, katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya vijijini, na ongezeko la watumiaji wa mitandao ya simu na huduma za mawasiliano ni kati ya fursa nzuri inayochangia ukuaji wa sekta ya fedha”, amesema Majaliwa.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema ameupitia mpango huo na kubaini kuwa umeainisha changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi hii katika harakati zake za kuongeza matumizi ya huduma za kifedha.
Katika hatua nyingine Mh. Majaliwa amewataka wajumbe wa Baraza la Taifa la Huduma Jumuishi za kifedha waaandae mpango mahsusi wa kutoa elimu vijijini kuhusu faida na umuhimu wa huduma jumuishi za kifedha Tanzania.
Comments
Post a Comment