Mahakama imemfutia kesi ya shambulio iliyokuwa ikimkabili Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima
Siku sita baada ya Adam
Malima kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mahakama imemfutia kesi ya
shambulio iliyokuwa ikimkabili.
Rais John Magufuli,
Alhamisi Oktoba 26,2017 alifanya uteuzi mbalimbali ukiwemo wa wakuu wa mikoa.
Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu leo Jumatano Novemba 1,2017 imeifuta kesi dhidi ya Malima na mwenzake.
Malima ambaye
amesharipoti mkoani Mara hakuwepo mahakamani wakati uamuzi huo ukitolewa.
Hakimu Mkazi Mkuu,
Respicius Mwijage ameifuta kesi hiyo na kuwaachia huru washtakiwa baada ya
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa kuomba ifutwe.
Chini ya kifungu cha 91
(1) cha Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, Mutalemwa ameomba shauri lifutwe kwa
sababu Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hana nia ya kuendeleza mashtaka dhidi ya
washtakiwa.
Baada ya ombi hilo
kuwasilishwa, Hakimu Mwijage alimuhoji Mutalemwa iwapo kuna sababu ya kuifuta
kesi hiyo na kama hana hataifuta.
Wakili Mutalemwa alisoma
kifungu hicho akisema kinampa mamlaka DPP kuiondoa kesi mahakamani wakati
wowote anapoona inafaa na pia, kinamruhusu kuirudisha mahakamani.
Baada ya maelezo hayo,
Hakimu Mwijage alikubali kuwaachia huru washtakiwa.
Shauri hilo lilikuwa katika
hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.
Waliposomewa maelezo ya
awali, Malima na mshtakiwa mwenzake Ramadhani Kigwande walikubali maelezo yao
binafsi, siku ya tukio walikuwepo Masaki, walikamatwa na kushtakiwa.
Walikana maelezo mengine
kuhusu mashtaka yanayowakabili.
Katika kesi hiyo, Malima
aliyewahi kuwa naibu waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne na mbunge wa zamani
wa Mkuranga alidaiwa Mei 15,2017 katika eneo la Masaki kwa makusudi alimzuia
ofisa wa polisi Konstebo Abdu kufanya kazi yake halali.
Comments
Post a Comment