MAHAKAMA HAINA RAFIKI
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amewataka viongozi wa vyama siasa kuacha tabia ya kufikilia vibaya Mahakama kuwa haiwatendei haki pindi wanapokuwa na kesi zao Mahakamani.
Polepole ameeleza hayo baada ya kushinda kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu ya mwaka 2015 kwa upande wa Ubunge katika jimbo la Longido Mkoani Arusha ambalo lilikuwa likigombewa baina ya Dkt. Steven Kiruswa kutoka CCM na Onesmo Nangole kutoka CHADEMA.
"Sisi kama chama cha Mapinduzi tumepokea uamuzi huo kwa faraja kubwa kwa sababu hivi karibuni kulikuwa na maneno kutoka kwa waakilishi wa vyama vya siasa vingine siyo vyote. Ambavyo vyenyewe huwa vinaamini kuwa Mahakama ikitoa haki kwao inakuwa imewatendea haki ila Mahakama ikitoa haki kwa wengine inakuwa haitendi haki. Sisi kama Chama cha Mapinduzi tunaamini Mahakama ipo pale ilipo kwa ajili ya kutenda na kutoa haki za watu wetu", alisema Polepole.
Aidha, Polepole amesema kwa upande wao wanaheshimu uamuzi uliyotolewa na Mahakama huku wakiomba Mahakama iendelee kufanya hivyo kila siku bila ya kujali itikadi ya chama husika.
"Kwa hiyo sisi huwa tunaheshimu uamuzi wa Mahakama na kwa uamuzi ambao umefanyika leo wa kutengua matokeo ya uchaguzi wa Ubunge katika jimbo la Longido, siyo tu kuwa umetupa faraja lakini sisi tunapenda kutoa rai kwa Mahakama iendelee kufanya kazi zake vizuri kwa uhuru, haki na isisikilize kelele za watu ambao huwa wanapenda Mahakama iseme nini ili ionekane inatenda haki. Kwa hiyo tutoe pongezi zetu kwa wananchi wa Longido na wana CCM kwamba madai yao ya haki kwamba Mahakama imeyathibitisha. Tuendelee kufanya siasa safi na tutoe uongozi bora lakini hatutakuwa tayari kuondolewa kwenye mstari, reli ya kutoa maendeleo kwa Watanzania", alisisitiza Polepole.
Kwa upande wake, Dkt. Steven Kiruswa amesema kwa mara ya nne Mahakama ya Tanzania imeweza kudhihirisha kwamba inaendeshwa kwa mujibu wa sheria na inajali kuhakikisha haki haipotei kwa muhusika.
Kwa mara ya kwanza kesi ya kupinga matokeo ya jimbo la Longido mkoani Arusha Novemba 11 mwaka 2015, majuma mawili kuisha tokea kumalizika kwa uchaguzi mkuu uliyofanyika Oktoba 25, 2015 ambapo Mahakama Kuu ya Arusha kwa mara ya kwanza ilibaini kuwa uchaguzi wa jimbo hilo haukuwa wa haki na kufikia June 6 mwaka 2016 Mahakama iliweza kutoa hukumu na kutengua Ubunge wa Onesmo Nangole na kupelekea jimbo hilo kuwa bila ya Mbunge yoyote kwa kipindi chote hicho kwa kuwa chama pinzani walikataa kurudia uchaguzi.BY EATV
Comments
Post a Comment