BOMBA LA MAFUTA GHAFI KUTOKA HOIMA MPAKA TANGA LITAITOA KIMASO MASO AFRIKA MASHARIKI
Rais Yoweri Museven |
WAKATI mchakato wa kuanza uchimbaji wa mafuta nchini Uganda ukishika kasi, Rais wa nchi hiyo, Yoweri Museveni amesisitiza kuwa sasa ni zamu ya nchi za Afrika Mashariki, ikiwemo Uganda, kukua, kuendelea na kufanya mapinduzi makubwa ya kiuchumi.
“Afrika Mashariki tuna kila kitu, hakuna kitakachotuzuia kupiga kasi katika maendeleo. Katika ukanda huu, hakuna mkulima wa kawaida atakayerithisha kazi ya kilimo kwa mwanaye, wakulima wanapaswa kuwa na watoto wasomi watakaoendeleza nchi hizi,” anasema.
Museveni amekuwa akiyarudia hayo mara kwa mara, na mara ya mwisho aliyasema hayo akiwa Tanzania mwanzoni mwa mwezi huu, wakati wa uzinduzi wa bomba la mafuta litakaloanzia Hoima, nchini Uganda hadi Chongoleani, nje kidogo ya Jiji la Tanga, Tanzania.
Bomba hilo, moja ya mabomba marefu ya mafuta duniani, linatarajiwa kugharimu Dola za Marekani bilioni 3.5 (zaidi ya Sh trilioni 7.5), linatarajiwa kukamilika mwaka 2020 na hivyo kuanza kuungana na nchi nyingine wazalishaji wa mafuta duniani.
Alisema licha ya mradi wa bomba hilo kuhusisha nchi za Tanzania na Uganda, lakini manufaa yake yatakuwa kwa nchi zote za Afrika Mashariki, kwani kuna uwezekano wa kunufaika nayo kwa njia nyingi, achilia mbali kwa usafirishaji wa mafuta pekee.
Ujenzi wa bomba hilo unaofanywa na kampuni za Total E&P, CNOOC na Tullow Oil kwa kushirikiana na Serikali za Uganda na Tanzania, utakuwa na urefu wa kilometa 1,445, kati ya hizo kilometa 1,149 likiwa katika mikoa minane na wilaya 24 za Tanzania Kilometa 296 tu zitakuwa za nchini Uganda.
Litakuwa na uwezo wa kusafirisha mapipa 216,000 kwa siku. Rais Museveni ambaye baada ya kurejea Kampala aliunda kamati kadhaa za kuharakisha mchato wa ujenzi wa bomba hilo na uchimbaji wa mafuta, alisema kutokana na Serikali ya Tanzania kuondoa tozo nyingi ili kufanikisha mradi huo, ana uhakika uzalishaji utakapoanza, Uganda itavuna pesa nyingi kama itakavyokuwa pia kwa Tanzania itakayotoza Dola za Marekani 12.5 (sh 26,500) kwa kila pipa.
Alisema manufaa hayatabaki kwa nchi hizo tu, bali Afrika Mashariki yote kwa ujumla, hivyo alizitaka nchi wanachama wa EAC kuuangalia mradi huo kama mali ya nchi zote, kwani kwa kadiri mafuta yanavyoendelea kugunduliwa katika nchi nyingine, kuna uwezekano wa baadaye nchi nyingine jirani zikatumia miundombinu hiyo kusafirisha mafuta katika nchi za Afrika Mashariki.
“Tayari kuna dalili upatikanaji wa mafuta Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Turkana, pia kuna uwekezano mkubwa wa kupatikana mafuta katika nchi za Rwanda, Tanzania na Burundi, hivyo naamini bomba hili litakuwa na manufaa makubwa,” alisema.
Katika hafla hiyo ya kihistoria, Museveni alisisitiza nchi za EAC zimebahatika kuwa na utajiri wa rasilimali zinazoweza kufanya mapinduzi makubwa ya kiuchumi katika ukanda husika, hivyo wananchi wake kuwa katika nafasi kubwa ya kuondokana na umasikini.
Alisema nchi za EAC zinapaswa kuachana na utamaduni wa kuzalisha vitu tusivyovitumia na kutumia tusivyovizalisha, akiongeza kuwa, vimechangia kuirudisha nyuma Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, huku wanaotoka nje ya Afrika wakinufaika zaidi.
”Tuna utajiri mkubwa, Afrika Mashariki hakuna kurudi nyuma tena,” alisema na kusifu misimamo ya marais wa zamani, Kwame Nkrumah wa Ghana na Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania katika kupigania haki za Waafrika.
Comments
Post a Comment